Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi ya kuzuia picha zako za faragha zisivuje
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Oktoba 2021, Mwanamuziki wa Afrobeats wa Nigeria, Tiwa Savage, alielezea kuhusu video yake ya faragha iliyovuja katika mitandao na kusema video hiyo iliwekwa kwa bahati mbaya kwenye Snapchat na mpenzi wake ambaye aliifuta baada ya kugundua lakini tayari ilikuwa imepakuliwa na mtu kwenye mtandao huo.
Katika nyakati hizi za teknolojia ya intaneti, usipokuwa mwangalifu na kile unachokiweka kwenye simu yako na kopyuta, unaweza kuingia katika majuto ya maisha yako yote. Kwa bahati mbaya kinachokwenda kwenye intaneti ni mgumu kukiondosha.
Kuna mamilioni ya watu kama Savage ambayo picha au video zao za faragha zimevuja kwa bahati mbaya au zimevujishwa kwa makusudi. Na ukweli usiopingika, kuna watu hupenda kuhifadhi picha na video zao za faragha katika vifaa vyao vya mawasiliano. Wakiwa na sababu mbalimbali za kufanya hivyo.
Kupiga picha za utupu ni uamuzi ambao ni ngumu kuuingilia. Lakini kile ambacho makala hii inakusudia kukigusia, ni ushauri wa namna ya kujilinda ili picha zako za faragha zisiende kwenye kadamnasi.
Usipige picha za utupu
Hii ndio kanuni ya kwanza, usipige wala kupigwa picha za utupu na kumtumia mtu au kuweka kwenye simu. Kinachoingia katika simu ni ngumu kukiondoka hata ikiwa utafuta. Kwa hivyo njia ya kwanza ya kujiepusha picha zako za faragha zisivuje, ni kuhakikisha hupigi kamwe picha za aina hiyo. Intaneti haina uhaba wa video au picha za aina hiyo.
Na punde tu unapoiweka picha yako kwenye simu, hiyo ndio hatua ya kwanza kuelekea picha hiyo kusambaa. Siku zote picha hizi huanza kwa kupigwa, kisha kutumwa kwa mtu au kuwekwa kwenye simu.
Usikubali kujirikodi kwa ajili na mtu mwingine. Wala usikubali kurikodiwa, hata ikiwa ni mpenzi, mume au mke wako. Hii ndio kanuni ya awali na muhimu kuliko nyingine zote, ili kuzuia faragha yako isiwe habari ya mjini katika mitandao ya kijamii.
Usionyeshe sura yako
Waswahili husema, ‘sikio la kufa halisikii dawa.’ Bilashaka kuna watu hawaambiliki hata kwa lugha gani. Watataka tu kupiga picha na kuhifadhi katika simu zao kwa sababu mbalimbali au kumtumia mtu.
Kuna chaguo namba mbili. Ikiwa kuna ulazima wa kupiga picha za aina hiyo, hakikisha sura yako haionekani. Iwe ni video, picha ya kawaida au mkutano kwa njia ya video (video call). Sura isionekane kwa namna yoyote ile.
Hii itakusaidia, ikiwa picha yako itaingia kwenye mitandao ya kijamii. Inaweza kuwa vigumu watu kujua ni picha ya nani. Itakuokoa na fedheha na aibu mbele ya marafiki, ndugu, wazazi na watu wako wa karibu.
Anayeshika simu yako
Simu yako inapokuwa na picha za aina hiyo, kuwa mwangalifu kuhusu nani anaishika. Baadhi ya picha huvuja kwa sababu simu imepelekwa kwa fundi au kushikwa na mtu ambaye baadaye anakusaliti.
Picha hizi ndizo ambazo hutumika katika kulipiza kisasi kutoka kwa mpenzi wako wa zamani, au kukulazimishwa ulipe pesa nyingi ili zisivujishwe. Kuna mifano mingi ya matukio ya aina hiyo, na mambo hayo wakati mwingine hufanywa na mpenzi uliyemuacha au fundi simu, ama kimada wa mwenza wako.
Usiamini watu kupita kiasi kuishika simu yako, ikiwa ina picha ambazo hutaki watu wengine wazione. Hata watoto, usiruhusu washike simu ikiwa kuna picha za ajabu ajabu, wanaweza kuzituma mitandaoni bila kukusudia.
Jichunge na wadukuzi
Faida yoyote ile unayoijua ya intaneti na simu, elewa kuna changamoto zake. Miongoni mwa changamoto za simu ni ule uwezo wa kudukuliwa, na unapaswa kuwa mwangalifu zaidi na watu wako wa karibu wanaoweza kuishika simu yako. Wapo wenye uwezo wa kuingilia simu yako.
Wanaweza kudukua mitandao yako ya mitandao ya kijamii kama WhatsApp na Facebook kwa kutumia mitandao mengine. Pia kuna uwezekano watu kuingia katika hifadhi ya simu yako na kutazama picha, jumbe fupi, video na kuzihamishia katika simu zao.
Jiepusha na watu wanaoomba picha za utupu kupitia mitandao ya kijamii kwa ahadi za kulipwa pesa. Usiingie kwenye mtengo wa namna hiyo. Biashara ya picha za utupu ni kubwa kwa sasa. Kuna watu wamejiajiri kwenye shughuli hizo na hufanya kazi masaa 24 kusaka picha za utupu.
Vilevile, jiepushe kuhifadhi picha zako za utupu katika mitandao. Huko ndiko ambako wadukuzi hufanikiwa kupenya ngome za mitandao mikubwa na kuchukua picha za watu bila wao wenyewe kujua.
Mwaka 2014 picha za utupu za watu maarufu katika tasnia ya burudani Marekani, zilivujishwa na wadukuzi ambao walifanikiwa kuvamia iCloud za simu za Apple. Bilashaka kuna maboresho makubwa kwa sasa, lakini ni muhimu kuwa macho.
Kuvuja kwa picha za utupu ni matukio ambayo hupelekea vifo. Wapo watu ambao picha zao zikivuja huingia kwenye msongo wa mawazo na hupelekea kujiuwa.
Toa taarifa
Katika baadhi ya nchi kuna mamlaka za serikali unazoweza kutoa taarifa juu ya kuvujishwa kwa picha zako, nao watakusaidia kuhakikisha zinaondoshwa. Cha kwanza, kusanya ushahidi wa picha hizo. Kwa Tanzania, toa taarifa katika Kitengo cha Polisi cha Makosa ya Mtandao (Tanzania Police Cybercrime Unit).
Pia unaweza kuwasiliana na kutoa taarifa katika majukwaa ambayo picha hizo zimesambazwa, ikiwa ni mitandao ya kijamii (Facebook, X, Instagram, YouTube, TikTok) au Google, ili kusaidiwa.
Mwaka 2021 pekee mtandao wa Reddit wenye makao makuu yake Marekani, jukwaa la watu kuzungumza, ulieleza kwa BBC kuwa, uliondoa picha 88,000 ambazo zilichapishwa bila ridhaa za wenyewe.
Fauka ya hayo, wasiliana na watu wenye ujuzi na utaalamu wa mambo ya mitandao. Zipo kampuni na wataalamu wa teknolojia, ni maalumu kwa ajili ya kutoa msaada katika kupambana na matukio ya namna hii.
Wakati mwingine mchakato wa kutoa taarifa na hadi picha kuondoshwa, huchukua muda au hugharimu pesa. Ndiposa, ile kanuni ya awali inabaki kuwa muhimu wakati wote, usipige wala usikubali kupigwa picha za utupu.
Ripoti ya shirika la FBI la Marekani ya mwaka 2026, imehitimisha kuwa, “imeona ongezeko kubwa la idadi ya visa vinavyohusisha watoto na vijana kushawishiwa na kulazimishwa kutuma picha chafu mtandaoni.”
Kwa kuhitimisha, ukiwa kama mzazi na mlezi, pia kuwa mwangalifu kuhusu watoto wako juu ya matumizi yao ya simu na kompyuta.