Ballon d'Or 2026: Nani ataibuka mshindi?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Macho ya mashabiki wa soka duniani leo usiku yanaelekezwa jijini London, nchini Uingereza, ambako washindi wa tuzo za Ballon d'Or za mwaka 2026 wanatarajiwa kutangazwa.

Hafla hiyo itafanyika katika ukumbi wa London Palladium, ikiwa ni mara ya kwanza kwa jiji la London kuandaa tuzo hizo katika historia yake ya miaka 70.

Tuzo za Ballon d'Or hutolewa kwa wachezaji wanaotambuliwa kwa kufanya vizuri zaidi katika soka duniani katika kipindi husika. Tuzo hizo huandaliwa na jarida la Ufaransa la France Football, kwa ushirikiano na Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA).

Nani anawania tuzo ya wachezaji bora?

Katika kipengele cha wachezaji wanaume, miongoni mwa walioteuliwa ni mshindi wa mwaka 2025, Ousmane Dembélé wa Paris Saint-Germain na Ufaransa, pamoja na Lionel Messi wa Inter Miami, Lamine Yamal wa Barcelona na Harry Kane wa Bayern Munich.

Wachezaji wengine walioteuliwa ni Kylian Mbappé wa Real Madrid, Erling Haaland wa Manchester City, Vinícius Júnior wa Real Madrid na Rodri, ambaye aliibuka mshindi mwaka 2024.

Kwa upande wa wanawake, orodha ya walioteuliwa inajumuisha Alexia Putellas na Ewa Pajor wa Barcelona, pamoja na Mariona Caldentey wa Arsenal na Barbra Banda wa Orlando Pride.

Mshindi wa tuzo ya wanawake mwaka 2025 alikuwa Aitana Bonmatí wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania.

Kinyang'anyiro kikali

Tofauti na miaka ya nyuma, msimu huu unatajwa kuwa na ushindani mkali zaidi, huku vigezo vya tuzo hiyo vikizingatia kiwango cha wachezaji kwa msimu mzima wa 2025–26 (kuanzia Agosti 3, 2025 hadi Julai 19, 2026) badala ya mwaka wa kalenda wa msimu wa soka

Wachambuzi wengi wa soka wanamtaja nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza na mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane, kama mchezaji anayepigia upatu mkubwa, wa kushinda tuzo hiyo.

Kane amekuwa na msimu mzuri wa ufungaji mabao nchini Ujerumani na barani Ulaya.

Hata hivyo, Kane anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa chipukizi wa Barcelona na Uhispania, Lamine Yamal, ambaye amewastaajabisha wengi kwa uwezo wake mkubwa uwanjani licha ya umri wake mdogo.

Nyota wa Real Madrid na Ufaransa, Kylian Mbappé, pamoja na viungo wa Uingereza Jude Bellingham na Declan Rice, pia wamo kwenye orodha fupi ya wachezaji 30 na wanatajwa kuwa na nafasi kubwa ya kuleta mshangao usiku wa leo.

Burudani na Sherehe

Mbali na kutoa tuzo kwa mchezaji bora wa kiume na wa kike, usiku wa leo utapambwa na burudani kutoka kwa wasanii wakubwa wa kimataifa kama Jorja Smith na French Montana, kuhakikisha kuwa sherehe hiyo inabaki kuwa ya kihistoria.

Je, Harry Kane atatunukiwa heshima hii kubwa baada ya miaka mingi ya ukame wa mataji, au kijana mdogo Lamine Yamal ataandika historia mpya? Majibu yote yatapatikana usiku wa leo huko London.

Historia ya tuzo za Ballon d'Or

Tuzo za Ballon d'Or zilianzishwa mwaka 1956 na jarida la France Football. Mshindi wa kwanza alikuwa mchezaji wa Uingereza, Stanley Matthews.

Mshindi wa tuzo ya wanaume anayeongoza kwa idadi ya tuzo hizo ni Lionel Messi, ambaye ameshinda mara nane huku Cristiano Ronaldo wa Ureno, mwenye tuzo tano, akiwa wa pili.

Vigezo vya kumpata mshindi

Washindi huchaguliwa kwa kura za waandishi wa habari za michezo kutoka nchi zinazostahili kushiriki katika mchakato huo.

Vigezo vikuu vinavyozingatiwa ni kiwango cha mchezaji binafsi, mafanikio ya timu yake na mwenendo wake wa kiuanamichezo pamoja na kuheshimu mchezo.

Mbali na tuzo kuu za wanaume na wanawake, hafla hiyo pia itatoa tuzo nyingine, zikiwemo za wachezaji chipukizi bora, makipa bora, makocha bora, vilabu bora na wafungaji bora.

Hafla ya mwaka huu itaongozwa na nyota wa zamani wa soka la Ufaransa, Thierry Henry, pamoja na mtangazaji wa michezo Kate Scott.