Moja kwa moja, Marekani na Iran zashambuliana kwa siku ya pili,afisa mkuu wa Iran asema "kukiuka makubaliano kutakuwa"na gharama

Marekani imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi ya anga dhidi ya Iran, huku milipuko ikiripotiwa katika maeneo ya kusini mwa nchi, ikiwemo karibu na Bandar Abbas na maeneo mengine ya pwani.

Skip Video and continue reading
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • xx
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Mariam Mjahid

  1. Iran yawasilisha malalamiko kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupinga mashambulizi ya Marekani

    Maeneo yaliyoshambuliwa

    Chanzo cha picha, Centcom

    Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema imewasilisha barua za malalamiko kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kufuatia mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani.

    Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Saeed Iravani, amesema Marekani imeanzisha tena "mashambulizi makubwa ya kijeshi dhidi ya mamlaka na mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," akidai kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa pamoja na wajibu wake chini ya sheria za kimataifa.

    Iravani pia alisema mashambulizi hayo yanakiuka kifungu cha makubaliano ya hati ya Maelewano ya Islamabad iliyosainiwa kati ya Iran na Marekani.

    Katika hatua nyingine, jeshi la Marekani limetangaza kuwa lilishambulia malengo 170 nchini Iran katika mawimbi mawili ya mashambulizi yaliyofanyika kwa siku mbili mfululizo.

    Katika ujumbe uliotumwa kupitia mtandao wa kijamii wa X, ukiambatana na video ya mashambulizi ya anga, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema lengo la operesheni hiyo lilikuwa "kuendelea kudhoofisha uwezo wa Iran wa kushambulia meli za kibiashara na mabaharia raia katika Mlango wa Hormuz."

    Kwa mujibu wa CENTCOM, mashambulizi hayo yalilenga mifumo ya ulinzi wa anga, vifaa vya ufuatiliaji na uangalizi wa maeneo ya pwani, maghala ya kuhifadhi makombora na ndege zisizo na rubani , uwezo wa vikosi vya majini, pamoja na miundombinu ya kijeshi na usafirishaji wa vifaa vya kijeshi katika ukanda wa pwani wa Iran.

    Unaweza kusoma;

  2. Mkuu wa NATO aiambia BBC kuwa matamshi ya Trump ni kama "mabishano ya kifamilia"

    Rutte (kushoto) amesema ana uhakika kwa asilimia 100 kuwa Trump ameendelea kujitolea kwa NATO.

    Chanzo cha picha, EPA

    Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, amesema muungano huo wa kijeshi wa mataifa ya Magharibi una nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

    Alitoa kauli hiyo katika mahojiano na BBC wakati wa mkutano wa kilele wa NATO uliofanyika mjini Ankara.

    Kauli hiyo imekuja licha ya matamshi makali ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye alisema amesikitishwa na kile alichodai kuwa NATO haikuungana na Marekani katika vita vyake dhidi ya Iran.

    Hata hivyo, NATO haikushirikishwa rasmi katika operesheni hiyo, ingawa baadhi ya nchi wanachama, ikiwemo Uingereza, ziliruhusu majeshi ya Marekani kutumia kambi zao kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya makombora ya Iran.

    Katika mahojiano hayo, mwandishi wa BBC alimwambia Rutte kuwa kuna tofauti kati ya kauli za matumaini zinazotolewa na viongozi wa NATO na matamshi ya wakati mwingine yanayoonekana kugawa yaliyotolewa na Trump.

    Katika mkutano huo, Trump alirudia msimamo wake kwamba Marekani inapaswa kuichukua Greenland na pia aliitaja Hispania kuwa "mshirika mbaya". Hata hivyo, alisema viongozi waliokutana Ankara walionesha umoja na kwamba kulikuwa na "upendo mkubwa" katika kikao hicho.

    Akijibu, Rutte alisema hali hiyo ni kama ilivyo katika familia.

    "Ni kama familia. Kuna familia ambazo hazigombani kabisa, na nyingine huzozana mara kwa mara, lakini bado hubaki familia," alisema.

    Rutte alisisitiza kuwa Trump anaendelea kuunga mkono NATO kikamilifu.

    "Trump ameijitolea kabisa NATO," alisema.

    Alipoulizwa ni kwa nini ana uhakika huo, ikizingatiwa kwamba Trump aliwahi kusema siku za nyuma kuwa kuiondoa Marekani ndani ya NATO ni jambo linaloweza kuzingatiwa, Rutte alijibu:

    "Nina uhakika kwa asilimia 100 kwamba Trump anaunga mkono NATO. Anaelewa kuwa operesheni za kijeshi za Marekani, ikiwemo Operesheni Epic Fury dhidi ya Iran, zisingeweza kufanyika kwa kiwango hicho bila kutumia Ulaya kama jukwaa la kuendeshea operesheni za kijeshi."

    Rutte alisema kuwa katika kipindi cha wiki sita kati ya mwisho wa Februari na katikati ya Aprili, kabla ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa, zaidi ya ndege za kijeshi 5,000 ziliondoka katika vituo vya kijeshi vya Ulaya kwa mujibu wa makubaliano ya pande mbili ya matumizi ya kambi hizo.

    Akizungumzia umuhimu wa nchi za Nordic zilizo wanachama wa NATO, ambazo ziko karibu na Rasi ya Kola nchini Urusi ambako kuna vituo vikubwa vya manowari zenye silaha za nyuklia, Rutte alisema eneo hilo lina mchango muhimu katika usalama wa Marekani kwa kutoa tahadhari za mapema kuhusu vitisho vinavyoweza kutokea.

    Unaweza kusoma;

  3. Trump asema Ukraine itapewa leseni ya kutengeneza makombora ya kujihami ya Patriot

    Zelensky

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema yuko tayari kuipa Ukraine leseni ya kutengeneza makombora ya kujihami ya Patriot, hatua ambayo inaweza kusaidia nchi hiyo kuimarisha ulinzi dhidi ya mashambulizi ya makombora ya masafa marefu kutoka Urusi.

    Akizungumza na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, wakati wa mkutano wa NATO uliofanyika Ankara Jumatano, Trump alisema: "Tutawapa leseni ya kutengeneza Patriot. Nafikiri wanaweza kuanza kuzalisha kwa haraka mara tu tutakapowapa maelekezo."

    Trump alisema bado hajawafahamisha watengenezaji wa mifumo hiyo ya ulinzi, kampuni za Lockheed Martin na Raytheon, kuhusu uamuzi huo, lakini aliongeza kuwa anaamini suala hilo litashughulikiwa vizuri.

    Mfumo wa Patriot hutambua na kuharibu makombora yanayolengwa angani na unachukuliwa kuwa miongoni mwa mifumo bora zaidi ya ulinzi wa anga duniani.

    Hata hivyo, pia ni miongoni mwa mifumo ghali zaidi, ambapo betri moja kamili yenye makombora yake hugharimu takriban dola bilioni moja za Marekani.

    Aidha, uzalishaji wake huchukua muda mrefu, huku takribani makombora 600 pekee yakizalishwa kwa mwaka, kwa mujibu wa wizara ya Ulinzi ya Marekani.

    Marekani imekuwa na tahadhari kuhusu kutoa mifumo hiyo kutokana na kuwa ilitumia zaidi ya nusu ya akiba yake ya makombora ya Patriot wakati wa vita vyake na Iran mapema mwaka huu, kwa mujibu wa taasisi ya utafiti ya Center for Strategic and International Studies (CSIS).

    "Tunayo mifumo ya Patriot, lakini si mingi. Tunaihitaji pia kwa ajili ya kujilinda sisi wenyewe," alisema Trump.

    Hata hivyo, Ukraine inahitaji kwa dharura mifumo ya ulinzi ya Patriot ili kujikinga dhidi ya mashambulizi ya Urusi.

    Katika miezi ya hivi karibuni, Moscow imeongeza mashambulizi ya makombora ya masafa marefu dhidi ya Ukraine, na kusababisha vifo vya watu kadhaa, hususan katika mji mkuu, Kyiv.

    Katika kipindi cha wiki iliyopita pekee, mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya makumi ya watu mjini humo.

    Unaweza kusoma;

  4. Rais wa Nigeria ataka kujua jinsi taasisi feki ilivyoanzishwa ndani ya ofisi yake

    Rais Tinubu

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma za ufisadi baada ya madai kwamba taasisi ya serikali isiyokuwepo kisheria iliundwa ndani ya ofisi yake na kupewa fedha za umma zenye thamani ya dola za Marekani 950,000.

    Kwa mujibu wa Ikulu ya Nigeria, barua iliyodaiwa kutolewa na Mkuu wa Wafanyakazi wa Rais ya kuanzisha Presidential Foreign Intervention Promotion Council (PFIPC) ilikuwa ya kughushi.

    Polisi wameanzisha msako dhidi ya Adeniyi Adeyemi Matthew, ambaye alikuwa akijitambulisha kama Mkurugenzi Mkuu wa PFIPC, kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kujifanya afisa wa umma na makosa mengine yanayohusiana.

    Kabla ya kutoweka, Adeyemi aliviambia vyombo vya habari vya nchini humo kuwa hana hatia na kwamba ana hofu kuhusu usalama wa maisha yake.

    Aliahidi kufika mahakamani kuthibitisha kutokuwa na hatia, akisisitiza kuwa taasisi hiyo ilianzishwa kwa mujibu wa sheria. Pia aliwashutumu baadhi ya maafisa waandamizi serikalini kwa kudai rushwa wakati wa mchakato wa uteuzi wake na baadaye kujaribu kudhibiti fedha za taasisi hiyo. Ikulu imekanusha tuhuma hizo.

    Adeyemi alisema PFIPC ilianzishwa mwaka 2024 kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa kigeni nchini Nigeria, lakini hakuna rekodi yoyote inayoonesha kuwa ilifanikiwa kufanikisha uwekezaji wowote.

    Taasisi hiyo ina wafanyakazi watatu pekee, ambao tayari wamehojiwa na polisi.

    Jumanne, Rais Tinubu aliiagiza Tume Huru ya kupambana na vitendo vya rushwa (ICPC) kufanya uchunguzi na kuwasilisha ripoti kamili ndani ya siku 30.

    Uchunguzi wa BBC News Pidgin umebaini kuwa taasisi hiyo ilikuwa imepata ofisi ndani ya Federal Secretariat, jengo kubwa la serikali linalohifadhi wizara nyingi za Nigeria katika mji mkuu, Abuja.

    Pia ilifungua akaunti za benki katika Benki Kuu ya Nigeria (CBN) na iliorodheshwa katika Sheria ya Bajeti ya mwaka 2026 ikiwa na mgao wa naira bilioni 1.3, sawa na dola za Marekani 950,000.

    Hata hivyo, Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali imesema PFIPC haikuwahi kuwa na akaunti inayofanya kazi katika Benki Kuu ya Nigeria, na haijawahi kupokea fedha za umma wala kulipa mishahara.

    Ikulu ya Rais imesema uchunguzi wa kisayansi uliofanywa na polisi umethibitisha kuwa saini ya Mkuu wa Wafanyakazi wa Rais, Femi Gbajabiamila, iliyokuwa kwenye barua inayodaiwa kuanzisha taasisi hiyo, ilighushiwa.

    Kwa mujibu wa mashtaka yaliyowasilishwa katika Mahakama Kuu, mjini Abuja, Adeniyi Adeyemi pamoja na washtakiwa wengine wawili wanatuhumiwa kutumia nyaraka za serikali zilizoghushiwa kuanzisha na kuendesha taasisi hiyo inayodaiwa kuwapo, kufungua akaunti kadhaa za benki kwa jina lake na kutafuta kutambuliwa rasmi kwa taasisi ambayo serikali inasisitiza kuwa haipo.

    Rais Bola Tinubu ameiagiza Tume Huru ya Kupambana na Vitendo vya Rushwa na Makosa Mengine Yanayohusiana (ICPC) kuchunguza tuhuma mbalimbali, zikiwemo:

    • Kughushi barua za uteuzi na nyaraka rasmi za serikali;
    • Kutumia madai ya uongo kutafuta utambuzi rasmi na uungwaji mkono wa kidiplomasia, ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa visa;
    • Kufungua akaunti nyingi za benki kwa kutumia nyaraka zinazodaiwa kughushiwa; na
    • Kuchunguza nafasi ya mtumishi yeyote wa umma, mtu binafsi, taasisi ya kifedha au mpatanishi ambaye huenda alihusika katika kuwezesha njama hiyo.

    Rais pia ameagiza wachunguzi kuchunguza mazingira yaliyoifanya taasisi inayodaiwa kuwa ya kubuniwa ionekane kuwa halali, pamoja na kubaini udhaifu katika mifumo na taratibu za serikali ambao unadaiwa kutumiwa kufanikisha mpango huo.

    Kashfa hiyo imezua shinikizo kubwa kutoka kwa mashirika ya kiraia, wanasiasa wa upinzani na mawakili waandamizi, ambao wamekuwa wakitaka kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu suala hilo.

  5. Mahakama ya ICC imesema imepata ushahidi katika uchunguzi wa uhalifu wa kivita nchini Sudan

    Makumi ya maelfu ya watu walikimbia mji wa El-Fasher baada ya kutwaliwa na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF).

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Maelezo ya picha, Makumi ya maelfu ya watu walikimbia mji wa El-Fasher baada ya kutwaliwa na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF).

    Naibu Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Nazhat Shameem Khan, amesema mahakama hiyo imepata "ushahidi thabiti" unaowahusisha viongozi wa kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF) na uhalifu wa kivita uliofanyika hivi karibuni katika jimbo la Darfur, Sudan.

    Akizungumza na BBC, Khan alisema ICC imepata "mafanikio makubwa" katika uchunguzi wake kuhusu mauaji ya raia yaliyotokea katika miji ya El-Fasher na El-Geneina.

    "Huenda ikachukua muda kabla haki haijapatikana na kesi kufikishwa mahakamani, lakini tutafika huko," alisema Khan, akiongeza kuwa ushahidi pia unawahusisha viongozi wa RSF na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

    Kuzingirwa na hatimaye kutwaliwa kwa mji wa El-Fasher kulikuwa miongoni mwa matukio mabaya zaidi katika vita vinavyoendelea kati ya RSF na jeshi la Sudan.

    Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 6,000 waliuawa mjini El-Fasher wakati RSF ilipouteka mji huo mwezi Oktoba mwaka jana.

    Aidha, kikundi hicho kinatuhumiwa kutekeleza mauaji ya halaiki kama hayo katika mji wa El-Geneina.

    RSF imeendelea kukanusha mara kwa mara tuhuma za kuhusika na mauaji ya watu wengi katika eneo lolote la Darfur.

    Hata hivyo, hakutaja ni lini mashtaka yanaweza kufunguliwa dhidi ya wale wanaodaiwa kuhusika na ukatili uliotekelezwa katika vita hivyo, vilivyoanza mwezi Aprili 2023.

    Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), yenye makao yake makuu mjini The Hague nchini Uholanzi, ni mahakama ya kimataifa yenye mamlaka ya kushtaki watu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.

    Khan alizungumza na BBC baada ya kutembelea kambi za wakimbizi mashariki mwa Chad, ambako watu waliokimbia mapigano huko Darfur walimweleza kuhusu ukatili walioupitia.

    Makumi ya maelfu ya watu walilazimika kuyahama makazi yao mjini El-Fasher, huku Umoja wa Mataifa ukisema kuwa ghasia zilizotokea huko zilikuwa na "viashiria vya mauaji ya kimbari."

    RSF imekanusha madai yaliyoenea kwamba mauaji yaliyotokea El-Fasher yalichochewa na misingi ya kikabila na kwamba yalifuata mtindo wa wanamgambo Waarabu kuwashambulia makundi yasiyo ya Kiarabu.

    Kikundi hicho kimesisitiza kuwa kiwango cha ukatili kilichoripotiwa kimezidishwa, ingawa kimekiri kwamba baadhi ya ukiukaji wa haki za binadamu ulitokea katika mji huo.

    Unaweza kusoma;

  6. Marekani yaanzisha mashambulizi zaidi dhidi ya Iran huku milipuko ikiripotiwa kusini mwa nchi

    Milipuko kadhaa iliripotiwa katika maeneo mbalimbali ya pwani ya Iran, ikiwemo miji ya Konarak na Chabahar.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Marekani imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi ya anga dhidi ya Iran, huku milipuko ikiripotiwa katika maeneo ya kusini mwa nchi, ikiwemo karibu na Bandar Abbas na maeneo mengine ya pwani.

    Maafisa wa Marekani wamesema mashambulizi hayo yanalenga kupunguza uwezo wa Iran wa kutishia usafiri wa majini katika Mlango bahari wa Hormuz, kufuatia mashambulizi yaliyodaiwa kufanywa na Iran dhidi ya meli za kibiashara.

    Iran imekosoa mashambulizi hayo na kuyataja kuwa ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, huku ikidai kujibu kwa kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Ghuba.

    Mvutano huo umeongeza hofu ya kuenea kwa mzozo katika Mashariki ya Kati na kusababisha bei za mafuta kupanda katika masoko ya dunia.

    Milipuko kadhaa iliripotiwa katika maeneo mbalimbali ya pwani ya Iran, ikiwemo miji ya Konarak na Chabahar.

    Televisheni ya taifa ya Iran imeripoti kuwa milipuko minane imetokea katika mji wa Bandar Abbas, huku ikidai kwamba makombora mawili yalipiga bandari za Sirik na Jask, ambazo zote ziko kusini mwa Iran.

    Vyombo vya habari vya serikali pia vilisema kuwa makombora mawili yalilipiga kisiwa cha Abu Musa, eneo ambalo limekuwa likizozaniwa umiliki kwa muda mrefu kati ya Iran na Falme za Kiarabu.

    Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya serikali ya Iran, mifumo ya ulinzi wa anga imewashwa katika mji wa Bandar Abbas kufuatia mashambulizi hayo.

    Kiwango halisi cha uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Marekani bado hakijajulikana. Hata hivyo, vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kukatika kwa umeme katika mji wa Chabahar na kuzuka kwa moto katika kambi ya Jeshi la Iran mjini Bushehr.

    Akizungumza na waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege ya rais, Air Force One, Jumatano jioni, Rais Donald Trump alisema Iran ilikuwa imewasiliana na Marekani muda mfupi uliopita na ilikuwa "inataka kufikia makubaliano kwa udi na uvumba."

    Trump aliongeza: "Sijui kama wanafaa kufanya makubaliano. Sijui kama watayaheshimu makubaliano hayo, hilo ndilo tatizo."

    Unaweza kusoma;

  7. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za leo