Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
CCM kuna Yuda au ni homa ya urais 2030?
Mitandao ya kijamii nchini Tanzania imelipuka kwa mjadala kuhusu jina moja tu - "Yuda". Ni jina ambalo limetamkwa mara nyingi katika siku mbili hizi, lakini bila kutajwa anayelengwa.
Aliyelirudisha jina hilo kwenye mjadala wa kitaifa ni Mbunge wa Tunguu, Zanzibar, Simai Mohammed Said. Akiwa Bungeni Dodoma wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Fedha, Simai alitoa kauli nzito kuhusu kile alichodai kuwa ni usaliti ndani ya CCM na Serikali. Akiwasilisha kwa kutumia fumbo la 'Yuda'.
Kauli hiyo ilizua maswali mengi kuliko majibu. Yuda ni nani? Kwanini Simai ameamua kuzungumza sasa? Na kwa nini achague Bunge, badala ya vikao vya chama, kuwasilisha ujumbe huo?
Lakini kadri mjadala wa "Yuda" ulivyozidi kushika kasi, swali kubwa zaidi likaanza kujitokeza. Je, Simai anazungumzia usaliti ndani ya CCM pekee, au amefungua pazia la mapambano ya urithi wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2030?
Hoja ya Simai – "Kumbe ni Yuda"
Simai Mohammed Said si mwanasiasa mpya ndani ya CCM. Kabla ya kuingia kikamilifu kwenye siasa, alikuwa mfanyabiashara aliyejikita katika sekta ya utalii.
Katika safari yake ya kisiasa, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini na ndani ya chama. Aliwahi kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, na baadaye Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar kabla ya kujiuzulu mwaka 2024, akieleza kuwepo kwa mazingira ambayo hayakuwa rafiki kwake kutekeleza majukumu yake.
Akiwa Bungeni, Simai alisema: "Kosa la mama ni wapi? Kwa sababu ya kumuamini mtu? Kumbe ni Yuda."
Kisha akaongeza: "Yuda huyu amesaliti ndugu zake, hata ile familia ambayo ilimlea kisiasa, hawataki kumuona huyu Yuda. Hata huko nyuma amewahi kutajwa ni mzigo, lakini leo mzigo huu tunao ndani ya Serikali."
Kwa mujibu wa Simai, mtu anayemzungumzia ameathiri wafanyabiashara, watendaji wa serikali na hata baadhi ya wanasiasa ambao safari zao za kisiasa zimekatizwa.
Lakini pamoja na uzito wa tuhuma hizo, hakumtaja mtu huyo kwa jina.
Fumbo la 'Yuda'
Katika simulizi za Kikristo, Yuda Iskariote anakumbukwa kwa jambo moja kuu - kumsaliti Yesu, licha ya kuwa mmoja wa wanafunzi wake wa karibu.
Ndiyo maana jina "Yuda" katika mazingira mengi ya kisiasa hutumiwa kuashiria usaliti, kutokuwa mwaminifu au kugeuka dhidi ya waliokujenga.
Simai hakufafanua moja kwa moja aliyekuwa akimlenga. Hata hivyo, kauli yake ilizua hisia kwamba ndani ya CCM kuna watu wanaoshukiwa kutokuwa waaminifu kwa misingi au historia ya chama.
Lakini kwa nini hoja hiyo imeibuka sasa?
Kwa wengi, muda wa kutolewa kwa kauli hiyo unaweza kuwa muhimu kuliko kauli yenyewe.
Wakati mjadala wa 'Yuda' ukiendelea, Mbunge wa ACT-Wazalendo, Addo Shaibu, alitoa tafsiri yake ya kisiasa kuhusu kinachoendelea. Tena aliitolea bungeni.
"Ninawaomba wabunge wa Chama Cha Mapinduzi, homa yenu ya siasa kuelekea 2030 isiharibu majadiliano ya Bunge hili."
Kauli hiyo ilihamisha mjadala kutoka kwa mtu mmoja anayejulikana kama "Yuda" na kuuelekeza kwenye swali la urithi wa kisiasa ndani ya CCM.
Rais Samia Suluhu Hassan, iwapo atamaliza mihula yake ya kikatiba, atahitimisha uongozi wake mwaka 2030. Hilo linaifanya mijadala yoyote kuhusu urithi wa kisiasa ndani ya CCM kutazamwa kwa jicho la tahadhari, hata kama hakuna mchakato rasmi ulioanza.
Wiki chache kabla ya kauli ya Simai, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wassira, naye aligusia jambo linalofanana.
"Nimeambiwa wengine wanazungumza urais wa mwaka 2030, leo? Tumemaliza uchaguzi mwaka jana, sasa si tujenge kwanza nchi?"
Kauli hiyo ilionekana kama onyo kwa wanachama au viongozi ambao tayari wanaanza kufikiria uchaguzi unaofuata wakati harufu na kumbuku ya uchaguzi wa 2025 hata bado haijapotea.
Kwa chama kilichozoea kuwa madarakani kwa miongo kadhaa, mijadala ya urithi wa uongozi huwa inaanza mapema zaidi kuliko inavyoonekana hadharani.
Kumbukumbu za 2015
Kwa wengi ndani ya CCM, uchaguzi wa mwaka 2015 unabaki kuwa mfano mkubwa wa jinsi ushindani wa ndani unavyoweza kuwa mkali, lakini pia jinsi ushindani huo unavyoweza kutikisa siasa za chama na taifa kwa ujumla.
Katika kipindi hicho, makundi mbalimbali yalijitokeza waziwazi. Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Lowassa alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliotajwa kuwa na ushawishi mkubwa kabla ya kuhamia upinzani baada ya kutopitishwa na CCM.
Kulikuwa pia na makundi yaliyomuunga mkono Hayati Bernard Membe, Waziri wa zamani wa mambo ya nje, huku mengine yakimuunga mkono John Magufuli ambaye hatimaye alipitishwa na kushinda urais dhidi ya Lowassa aliyekuja kuhamia upinzani, CHADEMA.
Miongoni mwa matukio yaliyokumbukwa zaidi ni kauli ya Emmanuel Nchimbi, ambaye sasa ni Makamu wa Rais, aliposema yeye pamoja na wajumbe wenzake wa Kamati Kuu ya CCM wakati huo, Sophia Simba na Adam Kimbisa, kwamba hawakukubaliana na baadhi ya maamuzi ya Kamati Kuu ya chama.
Ilikuwa ishara kwamba hata ndani ya chama chenye mfumo imara kama CCM, tofauti za maoni zinaweza kujitokeza wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais.
Mchambuzi wa siasa, Rehema Mema, anaamini nguvu ya CCM imekuwa katika uwezo wake wa kudhibiti tofauti za ndani bila kuathiri uimara wa chama kwa ujumla.
"Kitu kikubwa walichobarikiwa CCM ni kwamba hata kuwe na mgogoro wa aina gani, baada ya muda wanaweka sawa na mambo yanaendelea kama kawaida."
Historia ya CCM inaonyesha kuwa kila uchaguzi unapokaribia, makundi, majadiliano na hesabu za kisiasa huanza kujitokeza.
Ilikuwa hivyo mwaka 1995 wakati wa Benjamin Mkapa. Ikajirudia mwaka 2005 wakati wa Jakaya Kikwete. Na ikaonekana kwa nguvu zaidi mwaka 2015 wakati wa John Magufuli.
Ndiyo maana leo baadhi ya wachambuzi wanaona mjadala wa "Yuda" kama sehemu ya simulizi kubwa zaidi linalohusu mustakabali wa uongozi wa CCM.
Je, Simai alikuwa anazungumzia mtu mmoja anayemsadiki kuwa "Yuda" ndani ya CCM?
Au kauli yake imefungua dirisha la kutazama kile kinachoweza kuwa mwanzo wa hesabu za urais wa 2030?
Kwa sasa hakuna anayejua kwa uhakika. Lakini jambo moja liko wazi, ndani ya siku chache tu, neno "Yuda" limegeuka kuwa sehemu ya mjadala mpana zaidi kuhusu mustakabali wa uongozi ndani ya chama tawala.
Na huenda mjadala huo ukaendelea kwa muda mrefu zaidi kuliko kauli yenyewe.