Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
UFO ni nini na je, sayansi iko karibu kujibu kitendawili chake?
Mwezi Februari 1977 huko Pembrokeshire, Wales, mvua ikiwa inanyesha, wanafunzi wa shule ya msingi ya Broad Haven walidai kuona UFO (chombo cha angani kisichotambulika) nje ya shule hiyo.
David Davies, ambaye alikuwa na umri wa miaka 10 wakati huo, anasema anakumbuka marafiki zake wakijaribu kumtaarifu mkuu wa shule siku nzima kwamba kulikuwa na kitu cha ajabu kinachoendelea.
Davies alikuwa na uhakika kwamba kulikuwa na maelezo ya kimantiki kuhusu kile alichokiona.
"Lengo langu lilikuwa kutoka nje na kuthibitisha kuwa walikosea," anasema.
Lakini alipokwenda nje kuangalia kwa karibu zaidi, alieleza kuona "kifaa cha rangi ya fedha, chenye umbo la sigara, karibu na ukubwa wa basi, chenye sehemu ya juu iliyoinuka na taa nyekundu inayomulika juu yake."
Davies, ambaye alisema alikiona kitu hicho kwa takriban sekunde 10, alisema, "Nilihisi msukumo mkubwa wa kukimbia."
Tukio hili nchini Wales liliripotiwa kwenye programu ya BBC ya "Paranormal".
Mtaalamu wa anga akizungumza na BBC pia alisema kwamba kwa sasa, kutokana na uwepo wa simu na watu wengi kutumia programu za kufuatilia ndege, "tuko katika nafasi bora zaidi ya kufuatilia mambo yanayojulikana na yale yasiyojulikana."
Je, kuna sababu ya sisi kuziona UFO, na je, uzoefu kama huu unapaswa kuchunguzwa?
Uwindaji mwingi wa UFO
UFO zimekuwa zikivutia umakini wa watu wengi tangu madai ya kuona viumbe kutoka nje ya dunia huko New Mexico, Marekani, mwaka wa 1947.
Miaka mitatu baadaye, filamu Flying Saucer ilitolewa, na Mashindano ya Angani kati ya Marekani na Umoja wa Kisovyeti yalizidi kuimarika katika miaka ya 1950.
Hadithi za viumbe wa nje ya dunia zimeathiri utamaduni maarufu katika miaka iliyofuata, kutoka filamu iliyoshinda tuzo ya Oscar ya Steven Spielberg, E.T. mwaka 1982, hadi The X-Files, ambayo ilianza kuonyeshwa mwaka 1993.
Dkt. Ciaran O'Keeffe, mkuu wa sayansi ya jamii katika Chuo Kikuu cha Buckinghamshire , anasema kwamba hamasa ya kuona UFO ilifikia kilele katika miaka ya 1980, na kusababisha "uwindaji mwingi wa UFO."
Vyombo vya habari vya kimataifa viliripoti madai ya UFO, na tuhuma katika Shule ya Msingi ya Broad Haven.
Tukio la Broad Haven lilikuwa mojawapo ya madai kadhaa ya kuona viumbe kutoka nje ya dunia katika eneo linalojulikana kama Dyfed Triangle mwaka wa 1977. Nadharia kadhaa zimewahi kupendekezwa kuelezea maono haya, ikiwemo uwezekano kwamba ilikuwa ulaghai.
Ingawa kuona UFO kama lile la Broad Haven huvutia umakini mkubwa, Dkt. O'Keeffe anaamini kuna maelezo yanayowezakufafanua
"Ushuhuda wa mashahidi wa macho unaweza kukumbwa na makosa. Kumhoji shahidi kunaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa kumbukumbu yake kuhusu tukio hilo, hasa kama mahojiano hayafanywi kwa njia sahihi. Kwa mfano, maswali yanayoongoza mtu kutoa jibu fulani na hata namna vyombo vya habari vinavyowasilisha tukio vinaweza kuwa sababu zinazopotosha kumbukumbu."
Si kila kitu hutangazwa
Akizungumza katika programu ya Paranormal, mhandisi wa anga Dr. Ryan Marks anasema kwamba madai ya kuona UFO yanaweza pia kuelezwa na shughuli za anga, hasa katika maeneo ya mijini yenye viwanja vya ndege.
Kwa mujibu wa Makumbusho ya Jeshi la Anga la Kifalme ya Royal Air Force Museum, kulikuwa na viwanja vitano vya ndege Kusini mwa Wales kati ya 1970 na 1990, mojakikiwa kilitumika kama eneo la majaribio ya makombora.
Dkt. Marks anasema "Kulikuwa na msongamano wa mara kwa mara wa ndege, na uliongezeka zaidi miaka 40 iliyopita." Kulikuwa na kiwango fulani cha shughuli za kijeshi katika eneo hilo, na si zote zilikuwa zikitangazwa kwa umma.
Kwa mfano, kulingana na ripoti ya serikali ya Marekani ya Machi 2024, baadhi ya madai ya kuona UFO nchini humo katika miaka ya 1950 na 1960 yalitokana na ndege za kijasusi za kisasa na majaribio ya teknolojia ya anga.
Dkt. Marks anaeleza kwamba majaribio ya puto za hewa moto na ndege pia yalifanywa nchini Uingereza kuanzia katikati ya miaka ya 1970 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980, na kwamba baadhi ya majaribio hayo "yalifanana na maumbo yanayochorwa kama UFO."
Lakini pia anasisitiza kwamba haya yalikuwa "majaribio madogo" ambayo hayakuwahi kutoka nje ya anga.
Dkt. Marks anasema kwamba "msongamano wa ndege angani umerekodiwa na kuripotiwa kwa kiasi kikubwa, na ndege zinaweza kutambuliwa kwa urahisi kupitia programu za kuendesha shughuli za ndege.
Ila Davies bado anaamini kwamba aliona UFO.
"Kuwa na imani kuwa uliona UFO kunaweza kuonekana kama upuuzi," anasema.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilifunga kitengo chake cha UFO mwaka 2009, ikieleza kuwa hakikuwa na manufaa ya kiulinzi na kwamba wafanyakazi wake wanapaswa kuelekezwa kwenye majukumu ya ulinzi yenye thamani zaidi.