Makamu wa Rais Tanzania Emmanuel Nchimbi 'atangaza kujiuzulu'

Chanzo cha picha, Getty Images
Makamu wa Rais wa Tanzania, Emmanuel John Nchimbi, ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo na kustaafu siasa pamoja na utumishi wa umma, kwa mujibu wa barua inayosambaa mitandaoni.
Mpaka sasa hakuna mamlaka iliyothibitisha taarifa hiyo, ingawa BBC imezungumza na vyanzo vyake vya ndani serikalini vilivyothibitisha taarifa hiyo.
Vyombo vya habari vya ndani pia vimeripoti kuhusu taarifa hiyo ya kujiuzulu kwa Nchimbi.
Katika barua hiyo ambayo imechapishwa kwenye ukurasa rasmi wa Instagram wa Nchimbi, kiongozi huyo amesema amemwandikia Rais Samia Suluhu Hassan barua ya kujiuzulu.
Nchimbi ananukuliwa katika barua hiyo akisema kwamba uamuzi huo umefanywa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mujibu wa barua hiyo, auamuzi huo utaanza kutekelezwa Septemba 4, 2026.
Barua hiyo inasema wakati akiteuliwa kuwa Makamu wa Rais, alimuahidi Rais Samia kwamba angemsaidia kwa uwezo wake wote na kwa uaminifu. Na kwamba alimwahidi pia Rais kwamba endapo siku moja angeona anahitaji Makamu mwingine wa Rais, angeachia nafasi hiyo.
"Siku yoyote akiona anahitaji Makamu mwingine wa Rais, nitaacha nafasi hii.", Inasema sehemu ya barua hiyo.
Kwenye barua hiyo, Nchimbi ananukuliwa kwamba amejiridhisha kuwa Rais Samia anatamani mabadiliko, hivyo ameamua kutimiza ahadi hiyo.
Katika barua yake kwa Rais, Nchimbi amesema ameamua kustaafu siasa na utumishi wa umma.
Nchimbi amehudumu kama Makamu wa Rais kwa chini ya mwaka mmoja, tangu alipoapishwa kushika nafasi hiyo Novemba 3, 2025.
Alimrithi Philip Isdor Mpango, aliyekuwa Makamu wa Rais kati ya mwaka 2021 na 2025.
Kwa barua hiyo Nchimbi ananukuliwa akisema uamuzi wake wa kujiuzulu ni sehemu ya kutimiza ahadi aliyowahi kutoa kwa Rais kwamba angeachia nafasi hiyo iwapo Rais angeona anahitaji Makamu mwingine wa Rais.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na joto la ndani ya chama chake cha Chamapinduzi (CCM), na hata taarifa za kujiuzulu kwakwe zilianza kuzagaa kwa wiki kadhaa sasa.















