Kwa nini makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Iran na Marekani yamevunjika?

    • Author, Saeid Jafari
    • Nafasi, Political analyst
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Akiwa nchini Uturuki, Rais Donald Trump alitangaza kumalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran.

"Nadhani yamevunjika. Sitaki kuzungumza nao tena, ni wapumbavu," rais wa Marekani alisema kando ya mkutano wa kilele wa NATO huko Ankara.

Na mashambulizi yameanza tena kwa kiwango ambacho hakijaonekana tangu kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano (MoU) tarehe 17 Juni.

Washington na Tehran zinaonekana kuelekea kufufua tena mgogoro huo huku zote zikikataa kukubali kushindwa.

Shida ni kwamba Trump "hataki kukubali kushindwa kimkakati", anasema Robert Pape, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Chicago.

Karibu mambo yote yaliyochochea vita hivyo bado yapo, huku malengo yaliyotajwa na utawala wa Trump - kuanzia mabadiliko ya utawala, hadi makubaliano ya nyuklia na kudhoofisha mpango wa makombora ya balestiki wa Iran - hayajafikiwa.

Badala ya kupunguza ushawishi wa Iran, mzozo huo umeiinua Jamhuri ya Kiislamu na kufichua nguvu zake juu ya uchumi wa dunia kupitia udhibiti wa Mlango-Bahari wa Hormuz kwa uwezo wake wa kushambulia meli zinazopita.

"Kutokana na vita hivi, Iran imezidi kuwa na nguvu katika eneo hilo," anasema Pape.

Anayechukua nafasi ya kiongozi mkuu mwenye umri wa miaka 86 ni mwanawe mwenye umri wa miaka 56, Mojtaba Khamenei, huku uongozi wa Iran ukiwa na uwezo wa kuanzisha mashambulizi kwenye kambi za Marekani na kushambulia majirani zake wa Ghuba.

Baada ya wimbi la ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu ya Tehran kudhoofisha mwavuli wa usalama wa Marekani katika mataifa ya mafuta ya Ghuba, Saudi Arabia inaripotiwa kupanga mkutano wa maridhiano.

Makubaliano 14 yalitakiwa kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz na kupunguza bei kwenye soko la nishati duniani, huku yakizindua mazungumzo kuhusu swala tata zaidi la mpango wa nyuklia wa Iran na usaidizi wake kwa makundi ya wapiganaji ya kikanda.

Badala yake, kabla ya kushughulikia masuala ya nyuklia, tafsiri ya MoU yenyewe imekuwa uwanja wa ushindani, huku Tehran na Washington zikishindana kuweka masharti ya baada ya vita.

Ushindani huu unaweza kueleweka vyema kupitia maeneo matatu: Mlango-Bahari wa Hormuz, Lebanon, na mfuko wa ujenzi uliopendekezwa kwa Iran.

Mlango-Bahari wa Hormuz

"[Trump] hawezi kukubali Iran iwe na udhibiti wa Mlango-Bahari wa Hormuz," anasema Pape, akibainisha kuwa baada ya MoU kusainiwa, maafisa wa Marekani walianza "kujaribu kudhoofisha nguvu za Iran".

Kwa kufanya kazi na Oman, Marekani inatafuta kuanzisha njia mbadala ambayo haitegemei kupita Iran. Lakini Iran inasisitiza kuwa inasimamia Mlango-Bahari.

"Kwa mtazamo wa Tehran, makubaliano yalihusu kutotoza ada za usafiri wakati wa kipindi cha siku 60, bila kuacha jukumu lake la kusimamia mlango huo," anasema Hamidreza Azizi, mtafiti katika Taasisi ya Ujerumani ya Masuala ya Kimataifa na Usalama huko Berlin.

Washington inaweza kuongeza uwepo wake kijeshi au kuundwa kwa njia mbadala kama hatua za kudhibiti uhuru wa mlango huo. Lakini kwa Tehran, mlango-bahari ni muhimu kwa ushawishi wake wa kijiografia na kisiasa.

"Suala ni kwamba Iran inataka uwezo wake wa kusimamia njia hiyo kutambuliwa, kwa sababu ikiwa njia mbadala itaanzishwa bila idhini ya Iran, Tehran itaiona kama hasara ya kimkakati," anasema Azizi.

Kuhusu Lebanon

Mvutano kama huo unaonekana nchini Lebanon pia.

Ingawa MoU haisemi lolote kuhusu uhusiano wa Iran na makundi ya kikanda, ikiwa ni pamoja na Hezbollah, makubaliano hayo yanazitaka pande zote kusimamisha shughuli za kijeshi na kuhakikisha uhuru wa Lebanon. Masharti hayo mafupi hayakueleza kuondolewa kwa vikosi vya Israel.

Wachambuzi wengi walitafsiri kujumuishwa kwa Lebanon katika MoU kama moja ya mafanikio makubwa ya Iran, ikionyesha uhitaji wake wa kuona amani katika kanda yote.

"Hata hivyo, Marekani inaitafsiri hatua hiyo kama uthibitisho wa uhuru wa Lebanon na uadilifu wa eneo, bila kuipa Tehran jukumu lolote maalum katika mchakato wa kisiasa wa siku zijazo wa nchi hiyo," anasema Azizi.

Washington ilijaribu kupunguza kasi ya ushawishi wa Iran kwa kuanzisha mazungumzo ya kidiplomasia. Kwa mtazamo wa Tehran, kuharakishwa kwa mazungumzo yanayosimamiwa na Marekani kati ya Lebanon na Israel kunaweza kuonekana kama jaribio la kuitenga Iran.

Mfuko wa fedha

Pia bado haijulikani ni aina gani ya mfuko wa kifedha ambao Iran inaweza kuupata na ni masharti gani yanaweza kuunganishwa nayo, huku kukiwa na ripoti tofauti kuhusu kiwango na muda wa kuondolewa vikwazo na kuachiliwa fedha za Iran.

Jambo lenye utata zaidi ni tangazo la mfuko wa ujenzi wa dola bilioni 300 (£224bn), jambo ambalo liliwashtua hata wanasiasa wa Trump.

Wakati wa ziara yake ya Juni katika Ghuba, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio aliweka wazi kwamba uwekezaji wa pamoja nchini Iran unaendana na masharti kama vile mabadiliko juu ya programu za makombora na ndege zisizo na rubani za Iran na mabadiliko katika mwenendo wa Jamhuri ya Kiislamu katika eneo hilo. Hakuna hata moja kati ya haya lililoainishwa katika MoU ya awali.

Mbinu hiyo inaonekana ni kutumia uchumi kama njia ya kuchochea mabadiliko ya sera ya kigeni ya Iran.

Awamu mpya ya mgogoro?

Iran imeyatafsiri makubaliano hayo kama ushindi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi, aliviita vitisho vipya vya Trump "sio ishara ya nguvu, bali ni kukiri kushindwa kwa vikwazo, na vitisho, ambavyo havikuweza kuifanya Iran kupiga magoti".

Pande zote mbili zinaamini zinatetea msimamo wao, lakini hatua hizo hizo zinaweza kutafsiriwa kama kufungua awamu mpya ya mgogoro.

Pape, mwanasayansi wa siasa, anaelezea hali hii kama "mtego.”

Hormuz, Lebanon na hata mfuko wa uwekezaji unaonyesha kwamba Tehran na Washington bado ziko katika ushindani mkali, badala ya kuzingatia faida za pande zote na kupata njia mbadala ili kukwepa mzozo huu.