Ukoloni Afrika: Matukio kumi ya mauaji yaliyoacha maumivu makubwa

,l

Chanzo cha picha, (Picha na REPORTERS ASSOCIÉS/Gamma-Rapho via Getty Images)

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Ufaransa wakiwakamata raia wakati wa "Operesheni Bigeard" Machi 1956, wakati wa uasi huko Souk-Ahras, kusini mwa eneo la Constantine, nchini Algeria.
    • Author, Abdou Aziz Diédhiou
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 11

Baadhi wanaona shule, barabara, reli na miundombinu mingine, kama ndio matokeo pekee yaliyoachwa na makoloni ya Ulaya barani Afrika.

Wengi hawajui kwamba ukoloni wa Ulaya, uliotokea kati ya karne ya 19 na 20, pia uliambatana na vurugu, mauaji ya halaiki, unyang'anyi, kunyimwa uhuru na udhalilishaji wa utu kwa watu wa Afrika kabla ya uhuru wao.

Kuanzia Dakar hadi Nairobi, kutoka Algiers hadi Cape Town (Afrika Kusini), waliyoyapitia Waafrika chini ya utawala wa kikoloni yanafanana kutoka vurugu hadi ukatili wa majeshi ya kikoloni.

Kutawaliwa kwa nguvu, kulazimishwa kufanya kazi, unyang'anyi wa ardhi, uporaji wa rasilimali, matumizi ya vurugu za kutumia silaha pamoja na mauaji na uharibifu – yaliwakumba Waafrika.

Kiwango kamili cha mauaji haya ya kikoloni bado hakijabainishwa. Kinachojulikana ni kwamba katika baadhi ya nchi, watu waliuwawa ili kueneza hofu. Majeraha ya mauaji haya yanaendelea kuwa wazi katika nchi nyingi.

Katika makala haya, BBC inaangalia vurugu wakati wa ukoloni na mauaji kumi makubwa ya mataifa makubwa ya Ulaya kati ya 1850 na 1960 dhidi ya Afrika.

Senegal: Mauaji ya Thiaroye

l

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Makaburi zaidi ya 200 ya wapiganaji wa Senegal waliouawa Desemba 1, 1944 na Ufaransa katika kambi ya Thiaroye.

Idadi kamili ya waathiriwa wa mauaji haya mabaya bado haijulikani hadi leo. Serikali mpya ya Senegal unachimbaji katika eneo la kambi ya Thiaroye ili kujaribu kupata maelezo kamili ya mauaji haya yaliyofanywa na vikosi vya wakoloni wa Ufaransa mwaka 1944.

Desemba 1, 1944, katika kambi ya Thiaroye, yapata kilomita kumi na tano kutoka Dakar, mji mkuu wa Senegal, WaSenegal kadhaa walipigwa risasi na wenzao wa Jeshi la kikoloni la Ufaransa. Ni baada ya kudai malipo yao baada ya kushiriki vita.

Wapiganaji wa Senegal walikuwa miongoni mwa maelfu ya wanaume walioandikishwa katika makoloni ya Ufaransa ya Afrika ili kusaidia nchi hiyo katika vita vyake dhidi ya Ujerumani ya Nazi.

Kulingana na makadirio ya wanahistoria, jumla ya waathiriwa ni kati ya wapiganaji 300 na 400 waliouawa.

Makadirio haya yanatokana na ripoti kutoka kwa maafisa waliothibitisha kwamba zaidi ya wapiganaji 1,600 wa Kiafrika waliondoka Ufaransa Novemba 21, 1944, wakarudi Dakar baada ya vita.

Kulingana na baadhi ya wanahistoria, idadi ya waliouawa inafichwa kwa kutaja idadi ya waliouwawa kuwa ni 71.

Cameroon: Mauaji ya Kiekité 1956

m

Chanzo cha picha, /AFP kupitia Getty Images

Maelezo ya picha, Picha inaonyesha duka lililochomwa moto Juni 1960 huko Douala, wakati wa mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi wa Muungano wa Watu wa Cameroon (UPC).
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ni kazi ya wanahistoria wa Cameroon na Ufaransa wakiongozwa na Karine Ramondy ambao hivi karibuni walifichua kiwango cha ukandamizaji wa ukoloni wa Ufaransa nchini Cameroon.

Katika ripoti yao iliyowasilishwa kwa wakuu wa nchi hizo mbili Agosti 2025, wanahistoria wa Cameroon na Ufaransa wanaelezea mauaji ya Ekité.

Mauaji ya Ekité yalitokea usiku wa Desemba 30-31, 1956. Katika usiku huo, wanamgambo kutoka Umoja wa Watu wa Cameroon (UPC), chama cha kizalendo kilichodai uhuru, walikuwa wamekusanyika katika nyumba huko Ekité, mji ulioko kusini-magharibi mwa Cameroon.

Wengi wao walikuwa ni wapiganaji dhidi ya ukoloni tangu chama chao, kilichoanzishwa mwaka 1948, kuvunjwa mwaka 1955 kwa sababu ya msimamo wao wa uzalendo na kudai uhuru, na kulazimisha wanachama wake kujificha.

Hata hivyo, mkutano wenyewe katika makazi haya ulikuwa wa "amani,” anasema Karine Ramondy.

Badala ya kuingilia kati kuwakamata wanaharakati waliokusanyika, vikosi vya Ufaransa viliamua kuanzisha shambulizi, na kufanya mauaji ya kinyama kwa njia isiyo ya kawaida.

Idadi rasmi ya vifo ni 20 kwa mujibu wa Ufaransa, lakini ukweli ni uko tofauti na hivyo.

"Mashahidi wa eneo hilo wanazungumzia vifo vya watu 100 hadi 200, kwani wanaharakati kadhaa walikuwa wamekuja kushiriki katika mkutano huo muhimu," anasema Karine Ramondy.

Nchini Cameroon, jeshi la kikoloni la Ufaransa lilitekeleza mateso na mauaji dhidi ya wanamgambo wa UPC, akiwemo kiongozi Ruben Um Nyobè, ambaye aliuawa na jeshi la Ufaransa.

Kwa jumla, ukandamizaji wa Ufaransa dhidi ya wanamgambo wa UPC ulisababisha vifo vya takriban watu 7500 kati ya 1956 na 1962, kulingana na makadirio ya kijeshi.

Kulingana na wanahistoria ukandamizaji wa vikosi vya Ufaransa uliendelea hadi baada ya uhuru wa nchi hiyo Januari 1, 1960.

Emmanuel Macron pia alikiri mwaka 2025 kwamba Ufaransa ilianzisha "vita" nchini Cameroon kati ya 1945 na 1971, vita vilivyojaa "vurugu na ukandamizaji" dhidi ya raia.

Madagascar: Ukandamizaji na uasi 1947

k

Chanzo cha picha, /AFP kupitia Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ya tarehe Mei 1947 baada ya uasi wa Madagaska uliotokea mwaka 1947 na 1948 katika kisiwa cha Madagaska, ambacho wakati huo kilikuwa koloni la Ufaransa.

Wahenga husema, mtoto anapolia Madagascar kama unataka kumnyamazisha, unamwambia tu "Wasenegali wanakuja."

Ni kutokana na matendo yaliyofanywa na "wapiganaji wenye bunduki wa Senegal" walioandikishwa na jeshi la kikoloni la Ufaransa katika kampeni za "kutuliza" uasi katika kisiwa hicho kikubwa kati ya 1895 na 1947.

Machi 29, 1947, waasi walishambulia kambi ya kijeshi huko Moramanga, mji wa pwani ambapo waasi hao walifanya uasi dhidi ya ukoloni na uwepo wa Wazungu.

Ni uasi wa umma ulioongozwa na harakati za kizalendo ikiwa ni pamoja na MDRM (Harakati ya Kidemokrasia ya Malagasy) ambayo ilitetea mapambano dhidi ya ukoloni.

Uasi huo ulikandamizwa vikali na jeshi la kikoloni la Ufaransa. Ukatili na mauaji yalifanywa, na mauaji ya kiholela yalifanywa dhidi ya waasi waliokamatwa wakati wa uasi huu.

Mei 5 au 6, wanamgambo 166 wa MDRM waliofungwa walipigwa risasi kwenye mabehewa matatu yaliyofungwa. Walionusurika waliuawa kwa zamu na wapiganaji wa Senegal ambao walikuwa sehemu ya vikosi vya wakoloni.

Kwa jumla, idadi ya vifo kutokana na ukandamizaji inakadiriwa kuwa maelfu. Kati ya watu 30,000 na 40,000 waliuawa, kulingana na baadhi ya makadirio.

Congo: Mamilioni ya vifo chini ya Ubelgiji

km

Chanzo cha picha, Apic/Bridgeman kupitia Getty Images)

Maelezo ya picha, Mwaka 1900, kundi la wafungwa wameshikiliwa huko Congo kwa niaba ya wakoloni wa Ubelgiji waliotawala nchi hiyo. Makosa yao yalikuwa wizi na makosa mengine yanayofanana.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ya leo ilikuwa milki ya Leopold II wa Ubelgiji (1835-1909). Mfalme wa Ubelgiji alipewa sehemu ya Congo mwaka 1885 kufuatia Mkutano wa Berlin.

Alianzisha unyonyaji mkubwa kupitia mavuno ya mpira katika koloni hili lenye utajiri. Unyonyaji huu wa Congo ulisababisha mauaji ya watu, kupitia unyonyaji na kazi za kulazimishwa na utumwa.

Idadi ya waathiriwa ni milioni 10 kulingana na mwandishi wa Marekani Mark Twain.

1909, kitabu kinachoitwa ''Uhalifu wa Congo'' kilichapishwa na mwandishi na daktari Mwingereza Sir Arthur Conan Doyle, kikiangazia ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Congo chini ya Leopold II.

"Wengi wetu nchini Uingereza tunaona uhalifu uliotendwa katika ardhi ya Congo na Mfalme Leopold wa Ubelgiji na wafuasi wake kama uhalifu mkubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika historia ya wanadamu. Mimi binafsi naunga mkono maoni haya," aliandika Conan Doyle katika kazi yake.

Ivory Coast: Mauaji ya halaiki 1910

p

Chanzo cha picha, Prisma/UIG/Getty Images

Maelezo ya picha, Mchoro wa Machi 15, 1849 katika Pwani ya Ivory

Katika makala ndefu iliyochapishwa na Cahiers d'Etudes africaines, Fabio Viti, Profesa katika Chuo Kikuu cha Aix-Marseille, anajadili mauaji ya halaiki ya Diapé na Makoundié (Ivory Coast) ya Juni 1910 wakati ambapo Ufaransa ilikuwa ikijaribu kutuliza koloni hilo.

"Mnamo Juni 1910, mauaji mawili makubwa ya raia wasio na silaha yalifanyika siku tofauti, katika maeneo ya Abbey na Attié kusini-mashariki mwa Ivory Coast," aliandika Fabio Viti katika makala yake.

"Kwa miezi mitatu, watu wa Abbey, kwa kushirikiana na eneo jirani la Attié, walifanya uasi dhidi ya ukoloni wa Ufaransa. Kulingana na mtafiti huyo wa Kifaransa, uasi huo, ulilenga reli na maafisa wa kikoloni.

Kufuatia vitisho dhidi ya maafisa wa kikoloni, roho ya kulipiza kisasi ya maafisa wa Ufaransa na Wasenegali walioajiriwa na Ufaransa ilionekana wazi.

Ulipizaji kisasi ulisababisha vifo hamsini na vinne, wanaume ishirini, wanawake ishirini na wawili, wavulana wadogo 5, wasichana wadogo 7.

Wanaume watatu walikamatwa na kukatwa vichwa. Wengine walipigwa risasi na kisha kukatwa vichwa. Watoto waliuawa wakiwa wamelala kwa mama zao, wengine walipigwa risasi walipokuwa wakijaribu kutoroka," makala hiyo inaeleza.

Kenya: Waingereza dhidi ya Mau Mau 1950-1963

m

Chanzo cha picha, Getty Bettmann

Maelezo ya picha, Askari wakiwasindikiza wafungwa wakiwa wamebeba mabango yenye nambari Aprili 14, 1953 - Nairobi, Kenya

Mwaka 2011, Wakenya waliwasilisha malalamiko dhidi ya Uingereza katika Mahakama ya Haki za Kibinadamu ya Ulaya wakitaka haki ipatikane kwa ukatili waliotendewa na Waingereza wakati wa ukoloni.

Wanadai fidia ya dola bilioni 200 kwa uhalifu uliofanywa na Waingereza dhidi ya Mau Mau.

Machi 3, 1959, Wakenya 11 walifariki huko Hola karibu na Garissa, mashariki mwa Kenya, ambapo wanamgambo wa Mau Mau walikuwa wakishikiliwa.

Taarifa za awali kwa mujibu wa wananchi zilieleza kuwa waliwekewa sumu kwenye maji.

Lakini siku tatu baadaye, gavana wa Kenya, Evelyn Baring, alimwandikia Katibu wa Kikoloni, Alan Lennox-Boyd, kumwambia kwamba ripoti hizo ni za "kupotosha."

"Matokeo ya uchunguzi wa miili mitatu ya kwanza yanaonyesha kwamba, katika kila kisa, kifo kilitokana na vitendo vya vurugu," ilisema telegramu ya gavana kwenda London.

Katibu wa Kikoloni alianza kudai ripoti za kila siku kutoka Nairobi.

"Nina uhakika utaelewa hamu yangu ya kupata taarifa nyingi iwezekanavyo ifikapo asubuhi ya Jumanne, Machi 10," aliandika Bw. Lennox-Boyd.

Machi 9, Baring alituma telegramu hii London: ''Majeraha yanatokana na vipigo kwa fimbo nzito au rungu na/au buti''.

Nchini Kenya, watu wa Kikuyu, wakihisi kukandamizwa zaidi, walishiriki katika kampeni iliyolenga kupinga uvamizi wa wakoloni katika maeneo yao ya kilimo, kampeni hiyo ilisababisha kuibuka kwa harakati ya Mau Mau mwaka 1952 ambayo ilipigania uhuru wa kujitawala.

Kwa kujibu, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilituma rasilimali muhimu za kijeshi kukandamiza uasi huo, na kusababisha kukamatwa kwa maelfu ya Wakikuyu.

Simulizi kamili ya mauaji yaliyotokea wakati wa uasi wa Mau Mau nchini Kenya katika miaka ya 1950 iliwasilishwa katika Wizara ya Mambo ya Nje na kuwekwa hadharani.

Uasi wa Mau Mau katika miaka ya 1950 ulikuwa hatua muhimu katika mapambano dhidi ya uwepo wa Waingereza nchini Kenya.

Zaidi ya raia 1,800 wa Kenya waliuawa, na baadhi wanakadiria kwamba waasi wa Mau Mau wapatao 20,000 waliuawa.

Ukandamizaji wa Waingereza dhidi ya uasi huu ulisababisha kukamatwa kwa watu wengi wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa harakati ya Mau Mau, huku watu wengi wakinyongwa na Wakikuyu 150,000 wakifungwa katika kambi za kizuizini.

Moja ya matukio yaliyochochea mauaji zaidi ni uasi uliotokea Lari Machi 26, 1953, wakati wa mashambulizi yaliyofanywa na Mau Mau dhidi ya familia za Walinzi wa Kikoloni waliotii serikali ya kikoloni, na kusababisha vifo 74 na takriban majeruhi hamsini.

Mauaji haya yalisababisha kisasi na vurugu kutoka kwa Walinzi wa Kikoloni, walowezi, na vikosi vya wakoloni, na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Afrika Kusini: Kambi za njaa za Uingereza

l

Chanzo cha picha, Ann Ronan Picture Library/Universal Images Group kupitia Getty Images)

Mwishoni mwa karne ya 19, Afrika Kusini ilikuwa katika vita vya pili kati ya Waingereza na Makaburu (1899-1902), Makaburu ni wazungu wanaotokana na na kizazi cha walowezi wa Uholanzi waliofika mapema zaidi karne ya 17.

Ugunduzi wa dhahabu huko Transvaal, jimbo la Afrika Kusini mnamo 1886, jimbo lililokuwa likidhibitiwa na Makaburu, ulikuwa chanzo cha Vita vya Pili vya Makaburu.

Oktoba 1899, vita vilizuka kati ya Makaburu na vikosi vya Uingereza vilivyokuja kuwasaidia wahamiaji wa Kiingereza, vikiongozwa na Jenerali Frederick Roberts, kisha Lord Kitchener.

Kitchener alifuata sera ya ugaidi huko Transvaal. Alianzisha kambi zinazoitwa za "ulinzi." Mwishoni mwa 1901, wanawake na watoto 118,000 wa Kikaburu na watu weusi 43,000 walio waaminifu kwa makaburu waliwekwa katika kambi zipatazo arobaini ili "walindwe".

Lakini kwa kweli, kambi hizi ni kambi za vifo zenye uhaba wa chakula, uwepo wa magonjwa ya milipuko, surua, homa ya matumbo, kuhara damu na kusababisha kiwango cha juu cha vifo.

Inakadiriwa kuwa Makaburu 28,000, wakiwemo watoto 22,000, na kati ya watu Weusi 14,000 na 20,000 walipoteza maisha yao katika kambi hizi.

Septemba 1901, Lord Kitchener, katika ripoti kwa Ofisi ya Vita, aliandika: "Nchi ni shwari, na nimefanikisha hili bila umwagaji damu. Kambi za mateso, ambapo nimewakusanya wanawake na watoto, zinafanya kazi itakiwavyo."

Nigeria: Mauaji kwa ajili ya nyara

l

Chanzo cha picha, "Madhabahu iliyowekwa na mama malkia" (inayotoka Nigeria, Ufalme wa Benin, karne ya 18-19).

Maelezo ya picha, Kinyago kutoka Nigeria, wakati wa Ufalme wa Benin, karne ya 18-19.

"Benin ilizama katika janga," anaandika Barnaby Philips, mwandishi wa Loot - Britain and the Benin Bronzes, kitabu kinachosimulia uporaji katika ufalme huo wa Afrika uliofanywa na Waingereza.

Februari 1897, Waingereza walianzisha mashambulizi dhidi ya Ufalme wa Benin, uliokuweko Nigeria ya leo. Baada ya mapigano ya siku kumi, Waingereza walishinda. Mfalme aliondolewa madarakani, na moto mkubwa ukateketeza jiji.

Kulingana na Waingereza, asili ya shambulio hili lilikuja baada ya shambulio la kuvizia lililofanywa na wapiganaji wa ufalme mwezi mmoja mapema, ambalo lilisababisha vifo vya watu mia moja, akiwemo James Robert Phillips, kaimu balozi mkuu wa Ulinzi wa Pwani ya Niger.

Kuharibiwa kwa Ufalme wa Benin kulitokea wakati wa kipindi kinachojulikana kama "Kinyang'anyiro cha Afrika," ambapo mataifa saba ya Ulaya yalipambana ili kuteka sehemu kubwa ya bara la Afrika kadiri iwezekanavyo.

Benin ilikuwa ni ufalme uliostawi uliodhibiti biashara ya maliasili zenye thamani, kama vile mafuta ya mawese, pilipili hoho, matumbawe ya bluu na pembe za ndovu, ambazo zilikuwa na thamani sana kwa Waingereza.

Ushindi wa Uingereza uliripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa, ambavyo vilizungumzia "mahali pa kutisha," "mji wa damu," kama ilivyoripotiwa na New York Times, ikielezea matukio ambapo "watuhumiwa wa uchawi wa Ju Ju, au makuhani wa uchawi, walisulubiwa."

"Unyama" huu ambao kwa namna fulani ulihalalisha uingiliaji kati wa Uingereza, uligeuka kuwa mshangao wakati kazi za sanaa za shaba ambazo hapo awali zilipamba jumba la mfalme Oba zitakapofika Ulaya.

"Inawezekanaje sanaa nzuri kama hizi kuwepo katika jamii ya kikatili? waliandika wasimamizi wa Jumba la Makumbusho la Uingereza 1898 juu ya "Kazi za Sanaa za Jiji la Benin.”

Ukweli ni kwamba uzushi kuhusu ukatili kufanywa Benin, ndio ulisaidia kuhalalisha uvamizi na uporaji wa jumba la kifalme. Baadhi ya wanahistoria wanasema maelfu ya watu waliuawa katika shambulio hili.

Namibia: Mauaji ya halaiki ya Herero na Nama

l

Chanzo cha picha, PHILIP LITTLETON/AFP kupitia Getty Images

Ilikuwa nchini Namibia, nchi hii iliyo kusini mwa Afrika, ndipo mauaji ya kimbari ya kwanza ya karne ya 20 yalipotokea. Pia ni katika nchi hii ambapo Wajerumani walianzisha kambi za kwanza za mateso kabla ya kujenga zaidi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia kwa ajili ya Wayahudi, Waroma, na Wasinti.

Namibia ilikuwa koloni la Ujerumani. Akiwa ametumwa kuhakikisha utulivu wa eneo hilo jipya, Jenerali Lothar von Trotha alifanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Herero na Nama.

Utafiti umethibitisha kutolewa kwa amri ya kuangamiza watu aliyopewa Lothar von Trotha na Dola la Ujerumani 1904, ambayo ilisababisha mauaji ya watu wa asili wa Herero na Nama.

Kulingana na wanahistoria, mauaji haya ya kimbari yalisababisha vifo vya Waherero 65,000 hadi 70,000 na Wanama karibu 20,000, wakiwakilisha karibu 80% ya watu wa Waherero na nusu ya watu wa Nama, kati ya 1904 na 1908.

Mei 28, 2021 ndipo Ujerumani ilikiri kwa mara ya kwanza "kufanya uhalifu wa mauaji ya kimbari" nchini Namibia na kuomba msamaha.

Algeria: Mauaji ya Sétif, Mei 8, 1945

l

Chanzo cha picha, FERNAND PARIZOT/AFP kupitia Getty Images

Maelezo ya picha, Picha inayoonyesha gari lililoungua na maafisa katika mtaa mmoja nchini Algeria.

Huko Ufaransa, Mei 8, 1945, ilikuwa ndio mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia. Nchini Algeria, tarehe hii ndio mwanzo wa umwagaji damu huko Sétif.

Maandamano yanayowaleta pamoja watu wapatao 10,000 yanafanyika Setif siku ya mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia.

Algeria ilikuwa bado chini ya utawala wa Ufaransa. Kwa hivyo, waliandamana kupinga vita, na baadhi pia walikuwa na madai ya kutaka uhuru.

Walitaka mwisho wa utawala wa Ufaransa lakini pia kuachiliwa huru kwa kiongozi wa kizalendo, Messali Hadji, ambaye alikamatwa miezi michache nyuma.

Wakati wa maandamano hayo, mwanaume mmoja aliipeperusha bendera ya Algeria, ambayo ni bendera ya harakati za uhuru. Kuonyesha bendera hii hadharani ilikuwa marufuku.

Polisi walimpiga risasi mtu huyo na vurugu zinaanza. Wafaransa na Wazungu waliuawa. Ukandamizaji mkali unaoongozwa na Jenerali Duval ukatokea, kutoka kwa jeshi na wanamgambo.

Tume ya uchunguzi ilibaini idadi ya vifo ni kati ya watu 8,000 na 10,000. Wanahistoria wanakadiria idadi ya vifo kuwa kati ya 15,000 na 20,000.

Hata leo, historia hii chungu inaendelea kuchochea mvutano kati ya Algeria na Ufaransa.