Marekani itawezaje kuzuia meli za Iran katika Mlango-Bahari wa Hormuz?

l

Chanzo cha picha, EPA

    • Author, Jake Lapham
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Marekani imeanza kuzuia usafiri wa majini wa kuingia na kutoka katika bandari za Iran. Vikosi vya Marekani vinasema vitazuia au kurudisha nyuma meli zinazosafiri kwenda au kutoka pwani ya Iran.

Washington inasema meli zinazokuja au kutoka nchi nyingine zitaruhusiwa kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya maji ambayo Tehran iliifunga kutokana na mashambulizi ya Marekani na Israel.

Marekani itategemea meli zake za majini kudhibiti bandari za Iran, na hivyo kuzuia uwezo wa Tehran kufaidika na mauzo ya mafuta nje ya nchi katika jaribio la kuweka shinikizo kwa nchi hiyo.

Hii inakuja baada ya wapatanishi kutoka pande zote mbili kushindwa kufikia makubaliano ya kukomesha vita, ambavyo vilianza tarehe 28 Februari lakini kwa sasa nchi hizo ziko chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya wiki mbili.

Trump anataka kuweka shinikizo kwa Iran kwa kulenga shughuli mbili za kiuchumi – moja, ushuru mkubwa ambao Iran ilikuwa inautoza kwa meli ambazo zinapita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz, pili kuzuia mapato ya Iran kutokana na mauzo ya mafuta.

Rais wa Marekani aliiambia Fox News "hatutaiacha Iran ipate pesa kwa kuuza mafuta kwa watu inaowapenda na isiowapenda", akisema lengo ni kuruhusu meli zote kupita kwenye njia hiyo muhimu ya usafirishaji.

Iran imejibu kwa kuita kizuizi hicho "uharamia," ikitishia kisasi kwa kushambulia bandari katika mataifa ya Ghuba.

Mwandishi wa habari wa masuala ya usalama wa BBC Frank Gardner anasema kizuizi hicho kinaleta hatari mbili kuu:

  • Kitaongeza tena bei ya mafuta na gesi
  • Kusitishwa kwa mapigano kutavunjika, vita kamili vinaweza kuzuka tena kati ya Marekani na Iran, pia kuathiri maeneo kama Dubai, Bahrain, Kuwait na Saudi Arabia

Sheria zinasemaje

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kitabu cha mwongozo cha Kamandi ya Jeshi la Wanamaji la Marekani kuhusu sheria ya operesheni za majini kuanzia 2022 kinafafanua kizuizi kama "operesheni ya kivita ya kuzuia meli na/au ndege za nchi zote, adui na wasioegemea upande wowote, kuingia au kutoka bandarini, viwanja vya ndege, au maeneo ya pwani yaliyoainishwa ambayo ni ya, yanayokaliwa na, au chini ya udhibiti wa taifa la adui."

Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya baharini, limesema hakuna nchi yenye haki ya kisheria ya kuzuia usafirishaji wa meli katika njia zinazotumika kwa usafiri wa kimataifa.

"Ninaelewa kuna mgogoro unaoendelea, lakini bado hakuna msingi wa kisheria katika sheria za kimataifa wa kuchukua hatua za kuzuia njia yoyote inayotumika kwa usafirishaji wa kimataifa," anasema Katibu Mkuu wa shirika hilo Arsenio Dominguez.

Donald Rothwell, profesa wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia, anasema sheria za kimataifa zitaziona Marekani, Israeli na Iran kama maadui badala ya kuwa nchi 'zisizoegemea upande wowote'.

"Hii ina maana kwamba Marekani, kama adui, inaweza kuweka kizuizi halali chini ya sheria ya kimataifa - haswa, sheria ya vita vya majini," aliandika.

Kizuizi kitawekwaje?

Maeneo zilipo meli za jeshi la wanamaji la Marekani hayajulikani. Hilo linafanya iwe vigumu kujua hasa ni wapi Marekani itajaribu kuzuilia meli hizo.

Hata hivyo, jeshi la Marekani haliwezi kuweka meli zake za kivita karibu na pwani ya Iran kutokana na hatari ya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani.

Badala yake, lengo la kizuizi hicho huenda likawa ni karibu na Ghuba ya Oman, sehemu muhimu ya usafirishaji wa mafuta mengi duniani, ikiwa ni pamoja na mauzo ya nje ya Iran.

Vikosi vya Marekani huenda vikatumia satelaiti na taarifa za kiintelejinsia kufuatilia ni meli zipi zinazoondoka bandari za Iran, na kusubiri zisafiri hadi Bahari ya Hindi kabla ya kuzizuia.

Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) imesema zaidi ya meli 12 za kivita na zaidi ya ndege 100 za kivita na za ufuatiliaji zinahusika katika operesheni ya kuzuia meli za Iran.

Picha za setilaiti za tarehe 11 Aprili zilizochambuliwa na BBC Verify zinaonyesha meli ya kubeba ndege za kivita ya USS Abraham Lincoln ikiwa imesimama kwenye mashariki ya Ghuba ya Oman, takriban kilomita 200 (maili 124) kusini mwa pwani ya Iran.

Hii ndiyo meli ya kivita iliyo karibu zaidi na Ghuba ambayo BBC Verify imeiona tangu kuanza kwa vita.

Hadi sasa, hakuna meli zilizothibitishwa kukamatwa au kuzuiwa na Marekani.

Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) imesema itaruhusu meli za usafirishaji wa masuala ya kibinadamu ikiwemo chakula, vifaa vya matibabu na bidhaa zingine muhimu, ambazo zitakaguliwa.

Katika operesheni kama hiyo, Marekani ilitumia helikopta kushambulia meli za mafuta zinazoshutumiwa kufanya kazi kinyume cha sheria katika bahari ya Karibiani, lakini jeshi la Marekani halijatoa maelezo ya kutosha ikiwa itashambulia kwa helikopta meli za Iran katika eneo la Ghuba.

Trump pia amesema Marekani pia itaanza kuharibu mabomu yaliyo chini ya maji ambayo anayoituhumu Iran kuyaweka kwenye njia hiyo.

Katika taarifa mpya siku ya Jumanne, Centcom imedai kuwa meli sita za kibiashara zimeombwa kurudi katika bandari ya Iran kutoka Ghuba ya Oman.

Data ya ufuatiliaji wa meli iliyochambuliwa na BBC Verify inaonyesha kuwa meli mbili zinazohusishwa na Iran zilizosafiri kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz zimebadilisha mwelekeo na zinaonekana kurudi nyuma.

Inawezekana meli hizi zimetoa ripoti za uongo ili kuficha maeneo walipo.

Athari kwa Iran na nchi zingine

k

Chanzo cha picha, Marine Traffic

Maelezo ya picha, Usafiri ndani na karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz Aprili 10, 2026.

Kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, ambapo usafirishaji wa nishati duniani hufanyika, kumesababisha bei ya mafuta kupanda.

Lakini Iran imeendelea kuuza mafuta yake nje - na kwa kufanya hivyo, ilipata faida kutokana na bei kupanda. Machi ulikuwa mwezi wa tano kwa mauzo makubwa ya mafuta kutoka Iran katika mwaka mmoja na nusu uliopita.

Vizuizi hivyo vinaweza pia kuwa na athari kubwa kwa wateja wa mafuta ya Iran.

2022, karibu 82% ya mafuta ghafi na mafuta mengine yaliyotoka kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz yalielekea nchi za Asia, kulingana na Shirika la Taarifa za Nishati la Marekani (EIA).

China pekee inakadiriwa kununua karibu 90% ya mafuta ambayo Iran inasafirisha nje. Siku ya Jumanne, wizara yake ya mambo ya nje iliita kizuizi hicho cha Marekani kuwa cha "hatari" na "kisicho na maaana."

Wachambuzi wanasema kizuizi hicho kinaweza kuwa kimeundwa ili kuilazimisha Beijing kuihimiza zaidi Iran kuingia katika mazungumzo ya amani.

Kizuizi cha muda mrefu kinaweza kuharibu zaidi uchumi wa dunia, na kuongeza bei ya petroli na chakula, pamoja na kupunguza upatikanaji wa vifaa muhimu kama vile alumini, heliamu na akiba ya mbolea.

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) lilionya Jumanne kwamba uchumi wa dunia uko hatarini kudorora iwapo vita vitaendelea na bei za juu za nishati zitaendelea.

Meli ngapi hupita?

l

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Keir Starmer

Jiografia ya mlangobahari huo imeiruhusu Iran kuutumia kama mtaji wakati vita, ikitumia vitisho kuzuia vyombo vya maji kupita kwenye njia hiyo.

Takriban meli 3,000 kwa mwezi kwa kawaida husafiri kupitia mlango huo lakini idadi hii ilipungua sana wakati wa uhasama wa hivi karibuni.

Mlango huo pia ni njia muhimu ya kuingiza bidhaa Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na chakula, dawa na vifaa vya kiteknolojia.

Vizuizi vimesababisha mgogoro wa mafuta barani Asia, eneo linalotegemea sana mafuta ya Mashariki ya Kati.

Serikali zimewaamuru wafanyakazi kufanya kazi nyumbani, kupunguza wiki ya kazi, kutangaza likizo za kitaifa na kufunga vyuo vikuu mapema ili kubana matumizi.

Waziri Mkuu Sir Keir Starmer wa Uingereza amesema vikosi vya Uingereza havitashiriki katika kutekeleza vikwazo hivyo.

Meli za Uingereza za kutafuta mabomu ya chini ya maji na mifumo ya kupambana na droni vitaendelea kufanya kazi katika eneo hilo lakini meli za majini za Uingereza na wanajeshi hawatatumika kuzuia meli kuingia au kutoka bandari za Iran.

Trump amesema nchi zingine zitahusika katika kuziba mlango-bahari huo, lakini hakusema ni zipi.

Trump pia aliiambia Fox News kwamba Nato imejitolea kusaidia "kusafisha" njia hiyo, na kuongeza kwamba itakuwa tayari kutumika tena katika muda mfupi ujao.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi