Vita vya Sudan: Jumbe zamiminika kwenye simu ya mwandishi iliyozima kwa miaka mitatu

Chanzo cha picha, Mohamed Suleiman
- Author, Barbara Plett Usher
- Nafasi, Mwandishi wa Afrika
- Author, Mohamed Zakaria
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Muda mfupi baada ya Mohamed Suleiman kuingia katika ofisi ya mawasiliano ya simu katika mji wa pwani wa Port Sudan tarehe 13 Januari alianza kulia.
Hakuwa amesikia simu yake ikilia kwa muda mrefu tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, vilivyoanza miaka mitatu iliyopita kufuatia mzozo wa madaraka kati ya jeshi la nchi hiyo na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF).
Mwanahabari na msomi huyo alifika Port Sudan baada ya kunaswa katika mji wa magharibi wa el-Fasher, ambao kulitengwa na ulimwengu baada ya mawasiliano kukatizwa na kumfanya ashindwe kueleza kikamilifu maovu aliyokuwa akishuhudia.
"Nilichanganyikiwa kwa sababu watu walikuwa wakizungumza kwenye simu zao (ndani ya ofisi)," anaiambia BBC.
"Katika kipindi chote cha miaka mitatu iliyopita, simu yangu ilikuwa kimya. Baada ya kuingiza kadi, nilibubujikwa na machozi.''
Simu yangu ilipoanza tena kufanya kazi, ilikuwa na ujumbe wa takriban miaka mitatu, tathmini ya hasara iliyoshuhudiwa: habari za wafanyakazi wenzake waliokufa na marafiki wakiuliza ikiwa bado yu hai.
"Siku chache zilizopita, kuna mtu alinipigia simu akisema alidhani nimekufa," anasema. "Kuna watu walikuwa wamemwambia kuwa nipo Port Sudan, hivyo akanipigia simu, lakini hakuamini (ni mimi) hadi nilipompigia tena kwa njia ya video, ndipo alipoangua kilio."
Kwa kweli unaweza kusema ukimya ulikuwa karibu kuua kama vurugu, Suleiman anasema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Anaielezea kama "hisia ya kukosa hewa kwa sababu nilikuwa nikishuhudia mauaji yaliyofanywa kupitia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na mabomu au mauaji ya kikatili ya wakaazi wa el-Fasher na RSF kwa miezi 18.
Na hatimaye RSF ilipotwaa mji huo Oktoba mwaka jana, "Ilikuwa kama Siku ya Hukumu Duniani," anasema.
"Tulishuhudia Siku ya Kiyama Duniani."
Kuanguka kwa el-Fasher ilikuwa mojawapo ya sura za kikatili zaidi za vita vya wenyewe kwa wenyewe, vilivyoanza katika mji mkuu Khartoum tarehe 15 Aprili 2023.
Hivi karibuni ilienea katika maeneo mengine ya nchi na imekuwa mbaya sana katika eneo la magharibi la Darfur, ngome ya RSF, sehemu ilipo mji wa el-Fasher.
Wakati mzozo huo unaingia mwaka wake wa nne, mapigano yamesababisha mgawanyiko usio na kifani kati ya eneo linaloshikiliwa na jeshi na wanamgambo.
Mamilioni ya raia wa Sudan wametawanyika, wengine nje ya nchi, wakilazimishwa kutoka makwao katikati ya mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.

Chanzo cha picha, EPA
Juhudi za kidiplomasia za kumaliza vita vinavyoongozwa na Marekani hazijafaulu, huku pande zote mbili zikiungwa mkono na mataifa ya kikanda yenye nguvu ambayo yanaziwezesha kuendelea kwa mapigano.
Maelezo ya Mohamed Suleiman ni simulizi ya hali mbaya zaidi ya vita, na jinsi inavyoweza kuwaathiri watu wasio na hatia kwa kuwakosesha chakula, malazi, maisha na hata utambulisho.
Raia katika mji wa el-Fasher walinaswa katika mapigano kati ya RSF na makundi ya wenyeji yenye silaha ambayo yalisaidia jeshi kulinda mji huo. Wanamgambo walipozidisha udhibiti wao, shirika linaloratibu hali ya kibinadamu linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa likatangaza baa la njaa.
Kiwewe cha kila siku cha kifo na njaa kililipuka na kuwa matukio ya kusikitisha wakati watu walipojaribu kutoroka wakati wapiganaji wa RSF ilipokaribia.
"Tuliona watoto waliokufa mitaani," Suleiman anasema.
"Tuliona wanawake wakilia kutokana na njaa na kulemewa na kiu, walikuwa wadhaifu sana kiasi cha kushindwa kuwabeba watoto wao, hivyo wakawaacha njiani."
Kulikuwa na "watu tunaowajua kwa majina na tunaowajua baba zao, hatukuweza kuwasaidia na chochote".
"Hakuna chakula, hakuna maji, hakuna huduma ya kwanza ya kuwaokoa, au kuwasaidia. Huwezi kufanya chochote. Kwa hiyo unawakanyaga, kuwaruka, kulia, na kuendelea na safari," Suleiman anasema.

Chanzo cha picha, Reuters
Wengi walijaribu kukimbilia sehemu salama ya karibu kama vile mji wa Tawila. Barabara ilikuwa imejaa wafu na waliojeruhiwa - "walikuwa wengi sana, idadi isiyohesabika".
Kama kungekuwa na njia ya kuomba msaada, Suleiman anasema, wasingelazimika kuwaacha wengi waliojeruhiwa.
"Kuna mambo ambayo siwezi kuyaelezea kwa sababu yanapita maelezo, siwezi kuyazungumzia. Na jambo la kusikitisha ni kwamba vyombo vya habari vya sauti na taswira havikutoa tukio hilo.
"Hadi sasa, ulimwengu haujui kilichotokea katika mji wa el-Fasher, hata serikali haijui."
Uongozi wa RSF umekubali "ukiukwaji wa mtu binafsi" ulifanyika wakati wa unyakuzi wa el-Fasher lakini unasema haya yanachunguzwa na ukubwa wa ukatili ulitiwa chumvi na maadui wake. Pande zote mbili zinashutumiwa kwa uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na vifo vya raia kutokana na mashambulizi ya anga na ndege zisizo na rubani.

Chanzo cha picha, Reuters
Mawasiliano yalikuwa yameyumba sana jijini tangu mwanzo wa vita kwa sababu ya mapigano, na kwa sababu ya uhaba wa mafuta ambayo ilipunguza nguvu ya mitanpo. Hilo lilibadilika haraka ikaishia kukatika kwa umeme, Suleiman anasema, hali hiyo iliimarishwa wakati RSF ilipouzingira mji huo Mei 2024.
Baadhi ya watu walisafirisha kwa njia ya magendo katika vifaa vya Starlink vinavyowezesha muunganisho wa setilaiti kwenye intaneti. Lakini zilikuwa ghali sana na zilizuiliwa na jeshi wakati lilipochukua udhibiti wa jiji hilo.
RSF iliwanyang'anya chochote walichopata. Na waandishi wa habari waliofikia king'amuzi cha Starlink, walikabili hatari kubwa kutoka pande zote mbili, Suleiman anasema.
"Waasi wa RSF wanahisi kuwa una uhusiano na mashirika ya usalama na huenda wakafikiri unavitumia kufanya ujasusi," aliambia BBC.
"Kwa upande wa jeshi, wanaona kwamba wakati makombora yanapoanza, unatuhumiwa kutoa taarifa yanaelekea wapi," anasema, akimaanisha mtu anayeweza kutambua shabaha na kuwasilisha taarifa kwa adui.
"Dhana ya ujasusi ziliwaathiri wanahabari wengi na hivyo kuathiri uwasilishaji wa habari kutoka el-Fasher.
"Na mamlaka ya kijeshi haitoi kibali cha kuwasilisha ukweli. Kwa hiyo, unajificha, na unapojaribu kuwasilisha habari kisiri, unajiweka hatarini."
Suleiman pia alikabiliwa na hatari kama mtu mwingine yeyote.
Mnamo Julai 2025 mabaki ya kombora ilianguka chini ya mita mbili kutoka mahali alipokua akielekea nyumbani.
Alinusurika lakini alilala chini kwa takribani nusu saa huku akiwa ameshikilia simu ambayo hakuweza kupiga kuomba msaada.
"Kama ningejeruhiwa vibaya, nilingekufa," anasema.

Chanzo cha picha, Reuters
Aliona ndege zisizo na rubani zikipaa juu ya jiji lakini hakuwa na njia ya kuwatahadharisha watu ili waweze kujificha kutokana na mlipuko huo. Hata kutumia simu yake bila muunganisho wa mtandao kungemueka katika hatari ya kushambuliwa kwa sababu ya mwanga wa skrini.
"Wakati makombora yanapoanza, unajificha kwenye vyumba na chini ya vitanda. Au kwenye mfereji chini ya ardhi, au unajificha katika kitu chochote, wakati mwingine hadi saa saba katika hali ya hewa ya joto sana. Unakaa kimya, huwezi kuzungumza. Na huwezi kufikisha kile unachokiona."
Suleiman alishuhudia vifo vya watoto wengi, "hata wale waliokuwa kwenye mkokoteni iliyovutwa na punda, walishambuliwa kwa ndege isiyo na rubani".
Katoka hali kama hiyo, watu walielekeza imani yao kwa Mungu.
"Tulimkumbuka Mwenyezi Mungu usiku na mchana. Majirani walikuja pamoja kusoma Quran nyumbani," Suleiman anasema.
"Baada ya sala ya Alasiri, tulikuwa tunasoma sehemu ya Quran, huku ufyatuaji wa makombora ukiendelea. Ikiwa makombora yangetokea kaskazini, tungehamia kusini; yakipigwa kutoka upande wa kusini, tunahamia kaskazini."
Suleiman alimshukuru Mungu alipofika Port Sudan, makao makuu ya serikali inayoungwa mkono na jeshi kwa muda mwingi wa vita, Januari mwaka huu baada ya safari ya zaidi ya miezi miwili iliyompeleka Chad.
"Mara tu nilipofika Port Sudan, nilisujudu kwenye uwanja wa ndege na kulia sana kwa sababu sikuwahi kufikiria ningefika mahali salama," alisema.
Suleiman amefika salama, lakini hakuwa na hati zozote za utambulisho. Alipambana kuzipata tena na sasa anajihisi kama mtu tena ingawa ilikuwa kibarua kigumu cha kuthibitishe uraia wake.















